TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 24th Mei,2012
MKUTANO MKUU WA 28 WA ALAT - JUKWAA LA USHIRIKISHWAJI WA SEKTA BINAFSI
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) itakua na Mkutano Mkuu wa 28 tarehe 3 – 5 Mei 2012. Mkutano huo utafanyika hapa Dar es Salaam kwenye hoteli ya Kunduchi Beach.
Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 28 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ni “Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi”. ALAT imedhamiria kutumia Mkutano wake Mkuu wa Jumuiya kwa mwaka huu kuwa jukwaa la kupeana uzoefu wa ushirikiano baina ya sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP). Hii inatokana na sheria ya ubia iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania The Public Private Partnership (PPP Act) 2010. Mkutano huo ambao utafanyika tarehe 04- 05 Mei 2012, utatanguliwa na jukwaa la ubadilishanaji uzoefu juu ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi katika kutoa huduma kwa jamii na hasa katika kuzitumia Serikali za Mitaa. Ifahamike ya kwamba Serikali za mitaa sawa na majukumu yake, ndio zenye fursa ‘potential’ kubwa na nyingi za kutekeleza ubia kwa kufanya mashirikiano yenye manufaa na sekta binafsi. Jumuiya imeona haja na umuhimu wa kuandaa jukwaa hili kwa wanachama wake kwani ni lenye manufaa makubwa ya kuwafanya viongozi na watendaji wa Halmashauri zote nchini kuweza kujifunza na kufahamu dhana nzima lakini pia utendekaji halisi (Practicality) wa ubia. Hii pia ni fursa ya pekee kwa sekta binafsi, taasisi za Serikali na mashirika ya Umma kuweza kushiriki pamoja na viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kujadili jambo lenye manufaa kwa pande zote. Aidha Jumuiya inatoa nafasi chache za udhamini wa Mkutano Mkuu ambao pia utatoa fursa ya kushiriki moja kwa moja katika jukwaa hilo.
Jukwaa la ubadilishanaji uzoefu litakaloongozwa na mtaalamu aliyebobea wa kimataifa katika nyanja za ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP), litajadili mada mbalimbali zinazohusu ubia. Mada hizo ni pamoja na maana halisi ya ubia, je ni ubinafsishaji?; njia mbalimbali za kufanya ubia; msingi wa kisheria wa ubia, uzoefu wa halihalisi ya ubia kimataifa; dhati/dhamira hasa ya ubia; faida zinazoweza kupatikana kutokana na ubia; Mchakato wa ufanyikaji wa ubia na Uchaguaji wa miradi na upembuzi yakinifu. Mada nyingine ni Utambuzi wa viashiria vya hatari (risks) uchambuzi wake na upunguzaji; fursa za kifedha katika ubia; njia muafaka katika manunuzi; usimamizi wa ubia, uangalizi na tathmini.
Mkutano Mkuu wa kawaida wa Jumuiya hufanyika mara moja kila mwaka na wajumbe wake ni kama ifuatavyo: Wenyeviti na Mameya 133 wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya, Wakurugenzi 133 wa Halmashauri, Wabunge 21 mmoja toka kila mkoa. Mkutano huu utahudhuriwa pia na Wizara, Idara za Serikali Kuu, Wakala za Serikali, Taasisi shiriki katika Serikali za Mitaa, wawakilishi wa Balozi na Wabia katika Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za Serikali za Mitaa za Afrika Mashariki na wadau wangine wa sekta ya Serikali za Mitaa. Aidha Mkutano huu utahudhuriwa na Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika na Makampuni na Wawakilishi wa Sekta Binafsi. Inatarajiwa kwamba Mkutano huu utahudhuriwa na Washiriki takribani mia tano (500).
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ni chombo kinachoziunganisha Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji Tanzania Bara. Kwa sasa kuna Halmashauri 133 zinazounganishwa na chombo hiki.
Dira ya Jumuiya ni kuwa na Serikali za Mitaa zinazojitegemea na zenye ufanisi katika kutoa huduma zinazokidhi viwango kulingana na vipaumbele vya wananchi wake.
Mwelekeo wa Jumuiya ni kutambulika kama chombo na sauti ya pamoja ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ikitoa huduma za kitaalamu na kiufundi kwa wanachama wake.
Katika mkutano huo Jumuiya imemwalika Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgeni rasmi
Aidha watu mashuhuri wakiwemo viongozi wa Serikali na Sekta binafsi wamealikwa kutengeneza jopo la wasemaji. Miongoni mwa wanaotarajiwa ni Mhe. Mustafa Mkulo Waziri wa Fedha, Mhe. William Ngeleja Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. kapteni Mstaafu George Mkuchika Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Gaudensia Kabaka Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Emanuel Nchimbi Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mhe. Profesa Ana Tibaijuka Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mhe. Ezekiel Maige Waziri wa Maliasili na Utalii. Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dr.Cyiril Chami, Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Shamsi Nahodha, Waziri wa Kilimo na Ushirika Mhe. Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mifugo Dr. Mathayo David Mathayo. Walioalikwa wengine ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini Bwana Hari Kitilya, Inspekta Jenerali wa Polisi Ndugu Saidi Mwema Bi Esther Mkwizu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Huduma za Manunuzi Dr. Ramadhani Mlinga pamoja na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kwa namna ya pekee na kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais, Jumuiya imemwalika Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Fedha za Serikali (CAG) Ndugu Ludovick Utouh ambaye atawasilisha Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Fedha za Serikali za Mitaa.