TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO MKUU WA 30 WA ALAT - TANGA
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) itafanya Mkutano wake Mkuu wa 30 tarehe 7 – 10 Mei 2014. Mkutano huo unaodhaminiwa na benki ya NMB utafanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Regal Naivara Jijini Tanga. Kauli Mbiu ya Mkutano huu ambao pia utaanzisha mchakato wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 30 tangu kuanzishwa upya kwa mfumo wa Serikali za Mitaa hapa nchini na pia kuanzishwa kwa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) mwaka 1984 ni “Miaka 30 ya Serikali za Mitaa na
ALAT: Katiba Bila Sura ya Serikali za Mitaa ni Kudhoofisha Demokrasia ya Wananchi “.
Mkutano Mkuu wa kawaida wa Jumuiya hufanyika mara moja kila mwaka na wajumbe wake ni: Wenyeviti na Mameya 168 wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya, Wakurugenzi 168 wa Halmashauri, Wabunge 25 mmoja toka kila mkoa. Mkutano huu utahudhuriwa pia na Wizara, Idara za Serikali Kuu, Wakala za Serikali, Taasisi shiriki katika Serikali za Mitaa, wawakilishi wa Balozi na Wabia katika Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za Serikali za Mitaa za Afrika Mashariki na wadau wangine wa sekta ya Serikali za Mitaa. Aidha Mkutano huu utahudhuriwa na Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika na Makampuni na Wawakilishi wa Sekta Binafsi. Inatarajiwa kwamba Mkutano huu utahudhuriwa na Washiriki takribani mia tano (500).
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ni chombo kinachoziunganisha Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji Tanzania Bara. Kwa sasa kuna Halmashauri 168 zinazounganishwa na chombo hiki.
(C) Hon. Dr. Didas Massaburi addressing journalists not in picture flanked (r) by Mr. Habraham Shamumoyo Exec. Secretary of ALAT |
Kutokana na maombi kutoka kwa wadau mbalimbali imedhamiriwa kwamba Mkutano Mkuu wa 30 ambao mwenyeji waki ni Jiji la Tanga, utatoa fursa ya kipekee ya kuendelea kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu na kuendeleza ushirikiano baina ya sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP). Aidha katika kulitekeleza hilo Mkutano wa 30 umeongeza siku zake kuwa nne ili kutoa fursa ya kutosha kwa wanachama na wadau mbalimbali kupeana uzoefu wa mambo mbalimbali yanayaohusu sekta ya Serikali za Mitaa, sekta ya fedha na biashara, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Aidha muundo wa Mkutano mkuu umepanuliwa zaidi katika kutoa fursa ya kufanya sambamba mikutano mingine midogo (parallel Sessions) ili kuwawezesha washiriki wa Mkutano waweze kuketi katika makundi yenye kutoa huduma za pamoja katika Serikali za Mitaa na kujadili kwa ufasaha zaidi mambo yanyowasibu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Aidha hii ni fursa nyingine kubwa na ya pekee kwa sekta binafsi, taasisi za Serikali na mashirika ya Umma kuweza kushiriki pamoja na viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kujadili jambo lenye manufaa kwa pande zote. Mikutano pacha itakayoongozwa na wataalamu waliobobea katika nyanja za kuimarisha uchumi katika ngazi ya Jamii (Local Economic Development), utoaji wa huduma bora kwa jamii na utunzaji wa mazingira katika miji.
NMB Bank handing over a dummy sponsorship cheque of Tsh150 million |
Maandalizi ya awali ya Mkutano huu yameshafanywa ikiwa ni pamoja na kuwaalika wanachama, Serikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Wafadhili na wadau mbalimbali. Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
-MWISHO-
________________________________________
Dr. Didas Massaburi – Mwenyekiti ALAT (T) na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment